Water,Soil and Environmental Conservation

Water,Soil and Environmental Conservation
Wadco-Tanzania for sustainable use of soil,water and environmental conservation

Sunday, December 10, 2017

UMUHIMU WA MISITU KWENYE VYANZO VYA MAJI

Bila kutunza misitu hatuwezi kupata maji.

Maji-Ralilimali iliyo chanzo cha maisha. Misitu ni chanzo chake.
Maji ni moja kati ya rasilimali muhimu sana ambayo chanzo chake ni misitu. Ni kitu muhimu kwa viumbe hai vyote katika kujihakikishia maisha. Umakini katika uratibu wa misitu ni muhimu sana ili kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana kwa kizazi kilichopo na kijacho. Kila mkusanyiko fulani wa maji yaliyohifadhiwa au kujikusanya kiasili (water reservoir) yanakuwa na chanzo fulani yaalikotoka na hapo yaamekuja kwa kufuata mkondo (hata kama ya mvua)
Kwani Maji Yanatoka Wapi?
Mvukizo kutoka makusanyiko makubwa ya maji mfano bahari hubeba unyevu unyevu ambao hutengeneza mawingu angani. Upepo kutoka baharini huweza kuyasukuma hayo mawingu  juu zaidi. Kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa mawingu na tofauti  za kimgandamizo mawingu huanza kudondoka kama mvua. Mara nyingi mvua huwa kubwa maeneo yenye misitu mikubwa kwasababu miti husaidia kuzuia upepo unaovuma kuyapeleka mawingu maeneo mengine.
Maeneo yote hasa yenye misitu ambako mvua zikinyesha maji huanza kufuata mikondo midogo midogo (runoffs) au kupitia mikondo ya ndani kutokana na uelekeo wa mwinuko (underground streams) kwenda maeneno ya kujikusanya (mto au mabwawa) huitwa catchment areas.
Jamii  yenye shida ya maji huishi kama watumwa.
Je Misitu na Matumizi Yake Hupunguza Upatikanaji wa Maji?
Misitu hutoa tathmini (determine) ya kiwango (quantity), kima (rate) na ubora (quality) wa maji yanayopita katika mikondo mbalimbali na baadaye kuhifadhiwa maeneo mbalimbali kama mabwawa. Pamoja na misitu kuwa chanzo cha maji, lakini huwa chanzo na makao ya rasilimali nyingine kama wanyamapori, kutunza uasili wa eneo (nature conservation), uvunaji wa mbao, uchimbaji wa madini, tafiti za kitaaluma, ufugaji nyuki, soko la mauapori, utalii na kujifurahisha.
Shughuli hizo zote wakati fulani huhusisha magari kuingia msituni hivyo kuchafua mazingira, kuongeza mmomonyoko wa udongo, kuharibu uoto na uchomaji moto. Wakati mwigine udongo unaoshika katika magurudumu ya magari huweza kuhamisha au kusafirisha fangasi wanaosababisha magonjwa kwa miti kutoka sehemu moja kwenda nyingine hivyo kuongeza uharibifu zaidi. Kuzuia uharibifu huu usitokee inatakiwa kuwe na mpango wa pamoja wa kuratibu na kuaendesha maeneo ya vyanzo vya maji (Integrated Catchment Management), mpango shirikishi na angalizi wa uratibu wa maji, aridhi, uoto na rasilimali nyingine.
Ukataji miti au uchomaji moto ovyo hupelekea uondoaji wa kudumu wa miti hasa yenye mizizi mirefu ambayo hutumia maji yaliyo chini ya aridhi. Kadiri mvua inavyonyesha maji mengi yatakuwa yanaingia chini ya aridhi bila kutumika hivyo kiwango cha maji chini ya aridhi kinaongezeka (ground water level rises) na kuyeyusha chumvichumvi ya aridhini. Maji ya aridhini ambayo sasa yatakuwa yenye chumvi, yanaweza kupanda hadi juu ya aridhi na kutengeneza maeneo ya aridhi yenye chumvi ( salt scalds) au kwenda hadi kwenye mabwawa na kuyafanya yawe na maji chumvi. Maji yakiwa na chumvi ni moja kati ya uchafuzi wa maji (Salinity is one of water pollution), hivyo kwa lugha rahisi, ukataji wa miti maeneo ya misitu inakonyesha mvua na maji kuelekea katika mabwawa (catchment areas) husababisha chumvi katika mabwawa husika. Umakini katika uratibu wa misitu, utapunguza tatizo hili.
Ukataji ya asili miti kwaajili ya kuchoma mkaa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu
Mmomonyoko wa Udongo
Mmomonyoko hutokea pale ambao udongo unaondolewa kwenye aridhi yake ya asili kwa maji au upepo. Hii hutokea wakati miti na uoto ulio juu ya aridhi umeondolewa. Aina ya mmomonyoko iitwayo splash erosion hutokea wakati matone ya mvua yanapopiga aridhi tupu na kumomonyoa aridhi kwa kuondoa udongo na kuacha vishimo vidogovidogo.
Mmomonyoko mkubwa zaidi hutokea maeneo yenye mteremko mkali, hii ni kwasababu maji hukimbia kwa kasi zaidi hivyo kubeba udongo kirahisi. Udongo ulio momonyolewa kutoka maeneo zinakonyesha mvua (catchment areas), hubebwa na maji hadi kwenye mikondo mikubwa ya maji, mito na baadaye kwenye mabwawa na mikusanyiko mikubwa ya maji. Huko huyafanya maji kuwa na tope jingi (muddy/ turbid) na kuua mimea inayopatikana humo na viumbe wa majini. Hili likiendelea kwa miaka kadhaa, tope huchukua sehemu kubwa ya mabwawa na hivyo kupunguza kiwango cha maji yanayohifadhiwa na bwawa husika.
Ni vyema kuhakikisha miti na uoto juu ya aridhi (ground cover) vinalindwa na kujihakikishia uthabiti wa udongo wa juu (top soil) ili kupunguza nguvu ya matone ya mvua kuifikia aridhi moja kwa moja na kumomonyoa aridhi kiurahisi zaidi. Uoto pia hupunguza nguvu ya maji yanayokimbia juu ya aridhi hasa karibu na maeneo ya kuhifadhi maji hivyo kupunguza mmomonyoko.
Barabara zilizojengwa vibaya kwa kuwekewa miinuko mikali, huweza kuongeza kasi ya maji, na kama mitaro yake haijajengwa basi udongo mwingi utamomonyolewa na tope kupelekwa kwenye  maeneo ya kuhifadhi maji.. Barabara zikijengwa vizuri kwa kuzingatia maeneo maalumu ya kutokea  maji (drainage structures) uweza kupunguza kasi ya maji na hivyo kupunguza mmomonyoko wa udongo.
Mmomonyoko wa udongo hupelekea tope kujaa kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji.
Moto na Ubora wa Maji
Je kuchoma moto maeneo ya misitu au vyanzo vya maji hupunguza ubora wa maji? Jibu ni NDIOOOOO!!!
Moto wa msituni mara nyingi huwa na nguvu sana, na wakati mwingine sio rahisi kuthibiti. Huathiri misitu, miji, maisha ya watu na mashamba. Mara nyingi aina ya moto huu watu huchoma maeneo ambayo hayajawahi kuchomwa kwa miaka mingi hivyo kuwa na kiwango kikubwa cha maganda, majani, miti iliyokufa na masalia ya uoto mchanganyiko ambavyo huwa ni kichochezi (ground fuel).
Baada ya moto kuunguza msitu, aridhi hubaki nyeusi na tupu. Kama baada ya moto itafuata mvua kunyesha, basi majivu yaliyotokana na moto yatachukuliwa na maji ya mvua kwenda kwenye mikondo mikubwa na baadaye kwenye hifadhi za maji. Pia ikiwa baada ya moto utafauata upepo mkali, basi utabeba mabaki ya uoto na majivu na kuyapeleka kwenye vyanzo vya maji. Na pia kama mvua kubwa itaendelea kunyesha kabla uoto haujaota tena (vegetation recovery) basi udongo utamomonyoka kirahisi na kubebwa hadi kwenye hifadhi za maji hivyo kuyachafua na kupunguza ubora wa maji.
Nini Tufanye sasa?
Natoa rai kwa watu wote tupige vita uharibifu wa misitu kwa:
Kutokata miti ovyo, bali kupanda miti mingi,
Kutochoma moto bila utaratibu na kuweka njia za moto ikiwa ni lazima kufanya hivyo,
Kutofanya kazi za uzalishaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kama kulima, kufuga n.k
Kuhakikisha mikondo ya kutolea maji inajengwa kwa kufuata utaratibu hasa wakati wa ujenzi wa miundombinu ya barabara,
Kutunga sharia ndogondogo zitakazo wabana wanaokiuka sera ya taifa ya utunzaji mazingira na vyanzo vya maji.
Kupendelea kutumia nishati mbadala zisizo haribu mazingira.
Wakati wewe unachezea maji na kuharibu vyanzo na miundombinu yake, tambua wapo watu hawana maji kabisa.


Hitimisho:
Suala la kulinda vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira kwa ujumla halihitaji mtu awe msomi wa darasani ili kujua umuhimu wake. Hata wazee wa zamani hawakwenda shule lakini waliweka sheria kali na vitisho kwa watu wanaoharibu mazingira ili kuhakikisha wanalinda rasilimali hii muhimu. Hii ndio imesababisha tumeikuta misitu ya hifadhi kama Nyumbanitu uliopo mkoani Njombe, ambao umetunzwa kiasili kabisa tangu na wazee wa zamani, lakini umekuwa kivutio na chanzo muendelezo wa uzalianaji wa viumbe hai (ecosystem). Anza wewe kuyalinda mazingira, kumbuka maji ni uhai na bila maji hakuna linaloweza kufanyika.!

Eng Nguki Herman. M (Irrigation & Water Resources Engineering)
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101


Marejeo: 
1.      Clark, S. 1988. Institutional and legal issues. In: Working Papers for the National Workshop on Integrated Catchment Management. University of Melbourne, 17-19 May, 1988.
2.      Commonwealth of Australia 2000. Co-ordinating Catchment Management: Report of the Inquiry into Catchment Management. House of Representatives Standing Committee on Environment and Heritage, Canberra.
Nakushukuru kwa kusoma katika blog hii ili kujipatia maarifa juu ya maji, kilimo na mazingira. Ukitaka kupata mada mbalimbali za kijamii, vijana na mahusiano, tembelea www.ngukiherman.blogspot.com