Ofisi za Bonde la Mto Pangani, mkoani
Kilimanjaro, imekiri kuwapo kwa ongezeko kubwa la migogoro kati ya wakulima na
wananchi wa kawaida inayosababishwa na uhaba wa maji.
Akizungumza na waandishi wa habari (5 Jan 2017), Ofisa wa
Bonde hilo, Mtoi Kanyawana, alisema migogoro ya maji imekuwa ikiongezeka siku
hadi siku kutokana na ukame kuyakumba baadhi ya maeneo nchini.
“Hadi sasa tumepokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali
ikiwamo katika vijiji 19 vya Wilaya ya Moshi, mkoani hapa vyenye wakazi zaidi
ya 56,000.
“Wananchi hao wanadai kukosa huduma ya maji ya kunywa na
matumizi ya nyumbani kutokana na uwepo wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa
Kirua Kahe.
“Changamoto kubwa inayosababisha vyanzo vingi vya maji
kuvamiwa na kuharibiwa vibaya na wananchi ni kutokana na kubadilika badilika
kwa uongozi wa maeneo ya vijiji, hali ambayo inasababisha mfumo wa matumzi ya
maji kubadilika.
“Hata hivyo, kwa sasa tupo katika mchakato wa kuainisha
na kuyapandisha hadhi baadhi ya maeneo ya vyanzo vya maji na kuyahifadhi
ili kuhakikisha vyanzo hivyo vinalindwa na tatizo la upungufu wa maji
linakwisha,” alisema Kanyawana.
Kwa mujibu wa Kanyawana, maeneo yote ambayo yanategemewa
kupandishwa hadhi na kuwa hifadhi, yatakuwa chini ya miliki ya bonde hilo na
jukumu la kusimamia maeneo hayo wataliacha kwa Serikali za mitaa na vijiji kwa
kushirikiana na jumuiya za watumia maji.
“Yapo maeneo ambayo ni vyanzo vya maji, tuna mpango wa
kuja kuyatangaza ili yajulikane rasmi ili wananchi ikiwamo wafugaji ambao
wataingia, waweze kuwajibishwa kisheria.
“Lakini pia, maeneo mengine ambayo yana vyanzo vya maji
husimamiwa na jumuiya za watumia maji ambazo zipo kisheria,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema suala la utunzaji wa mazingira
katika vyanzo vya maji ni jambo muhimu na si jukumu la ofisi za Bonde la Mto
Pangani peke yake.
Source// Mtanzania 6 Jan 2017
Bila maji hakuna watu. Hayana ladha lakini huishi tabasamu wakati wa kuyanywa. |
Kwa sisi wadau wa rasilimali maji lazima tukubali kuwa hali hii inakoelekea inazidi kuwa mbaya. Nimechukua habari hiyo ya mfano kwa mkoa wa Kilimanjaro, lakini hali ni tete sehemu nyingi sana za nchi yetu. Hapa hatujikiti tu kulaumiana lakini upungufu wa maji maeneo mengi umetokana na uharibifu wa mazingira, uvamizi wa vyanzo vya maji kwa kilimo n.k. Kwa bahati mbaya wavamizi wa vyanzo vya maji wamekuwa wakifumbiwa macho ilihali wanafahamika, na huenda ni watu wenye ushawishi kwa jamii au nyadhifa fulani.
Lazima jicho la tatu litumike kuangalia tunakoenda. Mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo nayo kwa kiwango kikubwa yamechagizwa na uharibifu wa mazingira yanatishia hali ya maisha ya kizazi kijacho. Ni kweli teknolojia nyingi zinazidi kuvumbuliwa ili kutumia nishati mbadala na rafiki kwa mazingira, lakini bado muamko wa jamii ni mdogo ama kutokana na ukosefu wa elimu, gharama za teknolojia au makusudi tu.
Hili lipo wazi na ndio maana ukienda baadhi ya maeneo ambako wametunza mazingira na wamejiwekea sheria kali za kuthibiti wahalibifu wa misitu na wavamizi wa vyanzo vya maji, hali ni nzuri sana kana kwamba wao sio wa nchi hii. Kumbe jamii sasa umefika wakati wa kubadilika na kuthamini mustakabali wa kizazi kijacho. Sio tu kuweka sheria, bali kuwa na ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha hakuna anayekiuka. Bila maji hakunamaisha.
Eng Nguki Herman (Rasilimali maji na umwagiliaji)
0763 639 101/0679 639 101
ngukiherman@ymail.com