Bila kutunza misitu hatuwezi kupata maji. |
Maji-Ralilimali iliyo chanzo cha maisha. Misitu ni chanzo chake.
Maji ni moja kati ya
rasilimali muhimu sana ambayo chanzo chake ni misitu. Ni kitu muhimu kwa viumbe
hai vyote katika kujihakikishia maisha. Umakini katika uratibu wa misitu ni
muhimu sana ili kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana kwa kizazi kilichopo
na kijacho. Kila mkusanyiko fulani wa maji yaliyohifadhiwa au kujikusanya
kiasili (water reservoir) yanakuwa na chanzo fulani yaalikotoka na hapo yaamekuja
kwa kufuata mkondo (hata kama ya mvua)
Kwani Maji Yanatoka Wapi?
Mvukizo kutoka makusanyiko
makubwa ya maji mfano bahari hubeba unyevu unyevu ambao hutengeneza mawingu
angani. Upepo kutoka baharini huweza kuyasukuma hayo mawingu juu zaidi. Kutokana na kuongezeka kwa ukubwa
wa mawingu na tofauti za kimgandamizo
mawingu huanza kudondoka kama mvua. Mara nyingi mvua huwa kubwa maeneo yenye
misitu mikubwa kwasababu miti husaidia kuzuia upepo unaovuma kuyapeleka mawingu
maeneo mengine.
Maeneo yote hasa yenye
misitu ambako mvua zikinyesha maji huanza kufuata mikondo midogo midogo
(runoffs) au kupitia mikondo ya ndani kutokana na uelekeo wa mwinuko
(underground streams) kwenda maeneno ya kujikusanya (mto au mabwawa) huitwa catchment areas.
Jamii yenye shida ya maji huishi kama watumwa. |
Je Misitu na Matumizi Yake Hupunguza Upatikanaji wa Maji?
Misitu hutoa tathmini
(determine) ya kiwango (quantity), kima (rate) na ubora (quality) wa maji
yanayopita katika mikondo mbalimbali na baadaye kuhifadhiwa maeneo mbalimbali
kama mabwawa. Pamoja na misitu kuwa chanzo cha maji, lakini huwa chanzo na
makao ya rasilimali nyingine kama wanyamapori, kutunza uasili wa eneo (nature
conservation), uvunaji wa mbao, uchimbaji wa madini, tafiti za kitaaluma,
ufugaji nyuki, soko la mauapori, utalii na kujifurahisha.
Shughuli hizo zote wakati
fulani huhusisha magari kuingia msituni hivyo kuchafua mazingira, kuongeza
mmomonyoko wa udongo, kuharibu uoto na uchomaji moto. Wakati mwigine udongo
unaoshika katika magurudumu ya magari huweza kuhamisha au kusafirisha fangasi
wanaosababisha magonjwa kwa miti kutoka sehemu moja kwenda nyingine hivyo
kuongeza uharibifu zaidi. Kuzuia uharibifu huu usitokee inatakiwa kuwe na
mpango wa pamoja wa kuratibu na kuaendesha maeneo ya vyanzo vya maji (Integrated Catchment Management),
mpango shirikishi na angalizi wa uratibu wa maji, aridhi, uoto na rasilimali
nyingine.
Ukataji miti au uchomaji
moto ovyo hupelekea uondoaji wa kudumu wa miti hasa yenye mizizi mirefu ambayo
hutumia maji yaliyo chini ya aridhi. Kadiri mvua inavyonyesha maji mengi yatakuwa
yanaingia chini ya aridhi bila kutumika hivyo kiwango cha maji chini ya aridhi
kinaongezeka (ground water level rises) na kuyeyusha chumvichumvi ya aridhini.
Maji ya aridhini ambayo sasa yatakuwa yenye chumvi, yanaweza kupanda hadi juu
ya aridhi na kutengeneza maeneo ya aridhi yenye chumvi ( salt scalds) au kwenda
hadi kwenye mabwawa na kuyafanya yawe na maji chumvi. Maji yakiwa na chumvi ni
moja kati ya uchafuzi wa maji (Salinity is one of water pollution), hivyo kwa
lugha rahisi, ukataji wa miti maeneo ya misitu inakonyesha mvua na maji
kuelekea katika mabwawa (catchment areas) husababisha chumvi katika mabwawa
husika. Umakini katika uratibu wa misitu, utapunguza tatizo hili.
Ukataji ya asili miti kwaajili ya kuchoma mkaa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu |
Mmomonyoko wa Udongo
Mmomonyoko hutokea pale
ambao udongo unaondolewa kwenye aridhi yake ya asili kwa maji au upepo. Hii
hutokea wakati miti na uoto ulio juu ya aridhi umeondolewa. Aina ya mmomonyoko
iitwayo splash erosion hutokea wakati matone ya mvua yanapopiga aridhi
tupu na kumomonyoa aridhi kwa kuondoa udongo na kuacha vishimo vidogovidogo.
Mmomonyoko mkubwa zaidi
hutokea maeneo yenye mteremko mkali, hii ni kwasababu maji hukimbia kwa kasi
zaidi hivyo kubeba udongo kirahisi. Udongo ulio momonyolewa kutoka maeneo
zinakonyesha mvua (catchment areas), hubebwa na maji hadi kwenye mikondo
mikubwa ya maji, mito na baadaye kwenye mabwawa na mikusanyiko mikubwa ya maji.
Huko huyafanya maji kuwa na tope jingi (muddy/ turbid) na kuua mimea
inayopatikana humo na viumbe wa majini. Hili likiendelea kwa miaka kadhaa, tope
huchukua sehemu kubwa ya mabwawa na hivyo kupunguza kiwango cha maji
yanayohifadhiwa na bwawa husika.
Ni vyema kuhakikisha miti
na uoto juu ya aridhi (ground cover) vinalindwa na kujihakikishia uthabiti wa
udongo wa juu (top soil) ili kupunguza nguvu ya matone ya mvua kuifikia aridhi
moja kwa moja na kumomonyoa aridhi kiurahisi zaidi. Uoto pia hupunguza nguvu ya
maji yanayokimbia juu ya aridhi hasa karibu na maeneo ya kuhifadhi maji hivyo
kupunguza mmomonyoko.
Barabara zilizojengwa
vibaya kwa kuwekewa miinuko mikali, huweza kuongeza kasi ya maji, na kama
mitaro yake haijajengwa basi udongo mwingi utamomonyolewa na tope kupelekwa
kwenye maeneo ya kuhifadhi maji..
Barabara zikijengwa vizuri kwa kuzingatia maeneo maalumu ya kutokea maji (drainage structures) uweza kupunguza
kasi ya maji na hivyo kupunguza mmomonyoko wa udongo.
Mmomonyoko wa udongo hupelekea tope kujaa kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji. |
Moto na Ubora wa Maji
Je kuchoma moto maeneo ya
misitu au vyanzo vya maji hupunguza ubora wa maji? Jibu ni NDIOOOOO!!!
Moto wa msituni mara nyingi
huwa na nguvu sana, na wakati mwingine sio rahisi kuthibiti. Huathiri misitu,
miji, maisha ya watu na mashamba. Mara nyingi aina ya moto huu watu huchoma
maeneo ambayo hayajawahi kuchomwa kwa miaka mingi hivyo kuwa na kiwango kikubwa
cha maganda, majani, miti iliyokufa na masalia ya uoto mchanganyiko ambavyo
huwa ni kichochezi (ground fuel).
Baada ya moto kuunguza
msitu, aridhi hubaki nyeusi na tupu. Kama baada ya moto itafuata mvua kunyesha,
basi majivu yaliyotokana na moto yatachukuliwa na maji ya mvua kwenda kwenye
mikondo mikubwa na baadaye kwenye hifadhi za maji. Pia ikiwa baada ya moto
utafauata upepo mkali, basi utabeba mabaki ya uoto na majivu na kuyapeleka
kwenye vyanzo vya maji. Na pia kama mvua kubwa itaendelea kunyesha kabla uoto
haujaota tena (vegetation recovery) basi udongo utamomonyoka kirahisi na
kubebwa hadi kwenye hifadhi za maji hivyo kuyachafua na kupunguza ubora wa
maji.
Nini Tufanye sasa?
Natoa rai kwa watu wote
tupige vita uharibifu wa misitu kwa:
Kutokata miti ovyo, bali
kupanda miti mingi,
Kutochoma moto bila
utaratibu na kuweka njia za moto ikiwa ni lazima kufanya hivyo,
Kutofanya kazi za
uzalishaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kama kulima, kufuga n.k
Kuhakikisha mikondo ya
kutolea maji inajengwa kwa kufuata utaratibu hasa wakati wa ujenzi wa
miundombinu ya barabara,
Kutunga sharia ndogondogo
zitakazo wabana wanaokiuka sera ya taifa ya utunzaji mazingira na vyanzo vya
maji.
Kupendelea kutumia nishati
mbadala zisizo haribu mazingira.
Wakati wewe unachezea maji na kuharibu vyanzo na miundombinu yake, tambua wapo watu hawana maji kabisa. |
Hitimisho:
Suala la kulinda vyanzo vya
maji na utunzaji wa mazingira kwa ujumla halihitaji mtu awe msomi wa darasani
ili kujua umuhimu wake. Hata wazee wa zamani hawakwenda shule lakini waliweka
sheria kali na vitisho kwa watu wanaoharibu mazingira ili kuhakikisha wanalinda
rasilimali hii muhimu. Hii ndio imesababisha tumeikuta misitu ya hifadhi kama
Nyumbanitu uliopo mkoani Njombe, ambao umetunzwa kiasili kabisa tangu na wazee
wa zamani, lakini umekuwa kivutio na chanzo muendelezo wa uzalianaji wa viumbe
hai (ecosystem). Anza wewe kuyalinda mazingira, kumbuka maji ni uhai na bila
maji hakuna linaloweza kufanyika.!
Eng Nguki Herman. M
(Irrigation & Water Resources Engineering)
Instagram:
@eng.ngukiwamalekela
Phone: 0763 639 101/ 0679
639 101
Marejeo:
1.
Clark, S. 1988. Institutional and legal issues. In:
Working Papers for the National Workshop on Integrated Catchment Management.
University of Melbourne, 17-19 May, 1988.
2. Commonwealth of
Australia 2000. Co-ordinating Catchment Management: Report of the Inquiry into
Catchment Management. House of Representatives Standing Committee on
Environment and Heritage, Canberra.
Nakushukuru kwa kusoma katika blog hii ili kujipatia maarifa juu ya maji, kilimo na mazingira. Ukitaka kupata mada mbalimbali za kijamii, vijana na mahusiano, tembelea www.ngukiherman.blogspot.com |