Water,Soil and Environmental Conservation

Water,Soil and Environmental Conservation
Wadco-Tanzania for sustainable use of soil,water and environmental conservation

Sunday, December 10, 2017

UMUHIMU WA MISITU KWENYE VYANZO VYA MAJI

Bila kutunza misitu hatuwezi kupata maji.

Maji-Ralilimali iliyo chanzo cha maisha. Misitu ni chanzo chake.
Maji ni moja kati ya rasilimali muhimu sana ambayo chanzo chake ni misitu. Ni kitu muhimu kwa viumbe hai vyote katika kujihakikishia maisha. Umakini katika uratibu wa misitu ni muhimu sana ili kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana kwa kizazi kilichopo na kijacho. Kila mkusanyiko fulani wa maji yaliyohifadhiwa au kujikusanya kiasili (water reservoir) yanakuwa na chanzo fulani yaalikotoka na hapo yaamekuja kwa kufuata mkondo (hata kama ya mvua)
Kwani Maji Yanatoka Wapi?
Mvukizo kutoka makusanyiko makubwa ya maji mfano bahari hubeba unyevu unyevu ambao hutengeneza mawingu angani. Upepo kutoka baharini huweza kuyasukuma hayo mawingu  juu zaidi. Kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa mawingu na tofauti  za kimgandamizo mawingu huanza kudondoka kama mvua. Mara nyingi mvua huwa kubwa maeneo yenye misitu mikubwa kwasababu miti husaidia kuzuia upepo unaovuma kuyapeleka mawingu maeneo mengine.
Maeneo yote hasa yenye misitu ambako mvua zikinyesha maji huanza kufuata mikondo midogo midogo (runoffs) au kupitia mikondo ya ndani kutokana na uelekeo wa mwinuko (underground streams) kwenda maeneno ya kujikusanya (mto au mabwawa) huitwa catchment areas.
Jamii  yenye shida ya maji huishi kama watumwa.
Je Misitu na Matumizi Yake Hupunguza Upatikanaji wa Maji?
Misitu hutoa tathmini (determine) ya kiwango (quantity), kima (rate) na ubora (quality) wa maji yanayopita katika mikondo mbalimbali na baadaye kuhifadhiwa maeneo mbalimbali kama mabwawa. Pamoja na misitu kuwa chanzo cha maji, lakini huwa chanzo na makao ya rasilimali nyingine kama wanyamapori, kutunza uasili wa eneo (nature conservation), uvunaji wa mbao, uchimbaji wa madini, tafiti za kitaaluma, ufugaji nyuki, soko la mauapori, utalii na kujifurahisha.
Shughuli hizo zote wakati fulani huhusisha magari kuingia msituni hivyo kuchafua mazingira, kuongeza mmomonyoko wa udongo, kuharibu uoto na uchomaji moto. Wakati mwigine udongo unaoshika katika magurudumu ya magari huweza kuhamisha au kusafirisha fangasi wanaosababisha magonjwa kwa miti kutoka sehemu moja kwenda nyingine hivyo kuongeza uharibifu zaidi. Kuzuia uharibifu huu usitokee inatakiwa kuwe na mpango wa pamoja wa kuratibu na kuaendesha maeneo ya vyanzo vya maji (Integrated Catchment Management), mpango shirikishi na angalizi wa uratibu wa maji, aridhi, uoto na rasilimali nyingine.
Ukataji miti au uchomaji moto ovyo hupelekea uondoaji wa kudumu wa miti hasa yenye mizizi mirefu ambayo hutumia maji yaliyo chini ya aridhi. Kadiri mvua inavyonyesha maji mengi yatakuwa yanaingia chini ya aridhi bila kutumika hivyo kiwango cha maji chini ya aridhi kinaongezeka (ground water level rises) na kuyeyusha chumvichumvi ya aridhini. Maji ya aridhini ambayo sasa yatakuwa yenye chumvi, yanaweza kupanda hadi juu ya aridhi na kutengeneza maeneo ya aridhi yenye chumvi ( salt scalds) au kwenda hadi kwenye mabwawa na kuyafanya yawe na maji chumvi. Maji yakiwa na chumvi ni moja kati ya uchafuzi wa maji (Salinity is one of water pollution), hivyo kwa lugha rahisi, ukataji wa miti maeneo ya misitu inakonyesha mvua na maji kuelekea katika mabwawa (catchment areas) husababisha chumvi katika mabwawa husika. Umakini katika uratibu wa misitu, utapunguza tatizo hili.
Ukataji ya asili miti kwaajili ya kuchoma mkaa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu
Mmomonyoko wa Udongo
Mmomonyoko hutokea pale ambao udongo unaondolewa kwenye aridhi yake ya asili kwa maji au upepo. Hii hutokea wakati miti na uoto ulio juu ya aridhi umeondolewa. Aina ya mmomonyoko iitwayo splash erosion hutokea wakati matone ya mvua yanapopiga aridhi tupu na kumomonyoa aridhi kwa kuondoa udongo na kuacha vishimo vidogovidogo.
Mmomonyoko mkubwa zaidi hutokea maeneo yenye mteremko mkali, hii ni kwasababu maji hukimbia kwa kasi zaidi hivyo kubeba udongo kirahisi. Udongo ulio momonyolewa kutoka maeneo zinakonyesha mvua (catchment areas), hubebwa na maji hadi kwenye mikondo mikubwa ya maji, mito na baadaye kwenye mabwawa na mikusanyiko mikubwa ya maji. Huko huyafanya maji kuwa na tope jingi (muddy/ turbid) na kuua mimea inayopatikana humo na viumbe wa majini. Hili likiendelea kwa miaka kadhaa, tope huchukua sehemu kubwa ya mabwawa na hivyo kupunguza kiwango cha maji yanayohifadhiwa na bwawa husika.
Ni vyema kuhakikisha miti na uoto juu ya aridhi (ground cover) vinalindwa na kujihakikishia uthabiti wa udongo wa juu (top soil) ili kupunguza nguvu ya matone ya mvua kuifikia aridhi moja kwa moja na kumomonyoa aridhi kiurahisi zaidi. Uoto pia hupunguza nguvu ya maji yanayokimbia juu ya aridhi hasa karibu na maeneo ya kuhifadhi maji hivyo kupunguza mmomonyoko.
Barabara zilizojengwa vibaya kwa kuwekewa miinuko mikali, huweza kuongeza kasi ya maji, na kama mitaro yake haijajengwa basi udongo mwingi utamomonyolewa na tope kupelekwa kwenye  maeneo ya kuhifadhi maji.. Barabara zikijengwa vizuri kwa kuzingatia maeneo maalumu ya kutokea  maji (drainage structures) uweza kupunguza kasi ya maji na hivyo kupunguza mmomonyoko wa udongo.
Mmomonyoko wa udongo hupelekea tope kujaa kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji.
Moto na Ubora wa Maji
Je kuchoma moto maeneo ya misitu au vyanzo vya maji hupunguza ubora wa maji? Jibu ni NDIOOOOO!!!
Moto wa msituni mara nyingi huwa na nguvu sana, na wakati mwingine sio rahisi kuthibiti. Huathiri misitu, miji, maisha ya watu na mashamba. Mara nyingi aina ya moto huu watu huchoma maeneo ambayo hayajawahi kuchomwa kwa miaka mingi hivyo kuwa na kiwango kikubwa cha maganda, majani, miti iliyokufa na masalia ya uoto mchanganyiko ambavyo huwa ni kichochezi (ground fuel).
Baada ya moto kuunguza msitu, aridhi hubaki nyeusi na tupu. Kama baada ya moto itafuata mvua kunyesha, basi majivu yaliyotokana na moto yatachukuliwa na maji ya mvua kwenda kwenye mikondo mikubwa na baadaye kwenye hifadhi za maji. Pia ikiwa baada ya moto utafauata upepo mkali, basi utabeba mabaki ya uoto na majivu na kuyapeleka kwenye vyanzo vya maji. Na pia kama mvua kubwa itaendelea kunyesha kabla uoto haujaota tena (vegetation recovery) basi udongo utamomonyoka kirahisi na kubebwa hadi kwenye hifadhi za maji hivyo kuyachafua na kupunguza ubora wa maji.
Nini Tufanye sasa?
Natoa rai kwa watu wote tupige vita uharibifu wa misitu kwa:
Kutokata miti ovyo, bali kupanda miti mingi,
Kutochoma moto bila utaratibu na kuweka njia za moto ikiwa ni lazima kufanya hivyo,
Kutofanya kazi za uzalishaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kama kulima, kufuga n.k
Kuhakikisha mikondo ya kutolea maji inajengwa kwa kufuata utaratibu hasa wakati wa ujenzi wa miundombinu ya barabara,
Kutunga sharia ndogondogo zitakazo wabana wanaokiuka sera ya taifa ya utunzaji mazingira na vyanzo vya maji.
Kupendelea kutumia nishati mbadala zisizo haribu mazingira.
Wakati wewe unachezea maji na kuharibu vyanzo na miundombinu yake, tambua wapo watu hawana maji kabisa.


Hitimisho:
Suala la kulinda vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira kwa ujumla halihitaji mtu awe msomi wa darasani ili kujua umuhimu wake. Hata wazee wa zamani hawakwenda shule lakini waliweka sheria kali na vitisho kwa watu wanaoharibu mazingira ili kuhakikisha wanalinda rasilimali hii muhimu. Hii ndio imesababisha tumeikuta misitu ya hifadhi kama Nyumbanitu uliopo mkoani Njombe, ambao umetunzwa kiasili kabisa tangu na wazee wa zamani, lakini umekuwa kivutio na chanzo muendelezo wa uzalianaji wa viumbe hai (ecosystem). Anza wewe kuyalinda mazingira, kumbuka maji ni uhai na bila maji hakuna linaloweza kufanyika.!

Eng Nguki Herman. M (Irrigation & Water Resources Engineering)
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101


Marejeo: 
1.      Clark, S. 1988. Institutional and legal issues. In: Working Papers for the National Workshop on Integrated Catchment Management. University of Melbourne, 17-19 May, 1988.
2.      Commonwealth of Australia 2000. Co-ordinating Catchment Management: Report of the Inquiry into Catchment Management. House of Representatives Standing Committee on Environment and Heritage, Canberra.
Nakushukuru kwa kusoma katika blog hii ili kujipatia maarifa juu ya maji, kilimo na mazingira. Ukitaka kupata mada mbalimbali za kijamii, vijana na mahusiano, tembelea www.ngukiherman.blogspot.com

Friday, April 14, 2017

MVUKIZO KATIKA UHIFADHI MAJI (EVAPORATION)


Mvukizo/Evaporation-Upotevu wa maji usioonekana kwa macho

Mvukizo au Evaporation kwa kingereza ni hali ya maji kubadilika na kuwa katika maada ya gesi.. Ili hii kutokea ni lazima nishati nyingi na mgandamizo wa hewa uwepo, na ndio maana mvukizo huwa mkubwa kwenye maeneo yenye joto kali.. Mvukizo hurudisha sehemu ya maji iliyoshuka kama mvua moja kwa moja  katika angahewa (atmosphere) kabla hayajatumika kwa shughuli yoyote.

Mvukizo/Evaporation inatokea kuanzia muda mchache baada ya mvua kukatika hadi kwa kipindi cha msimu mzima (whole season). Kama ilivyo katika mvua, mvukizo pia hupimwa kwa kizio cha milimita chini ya muda fulani kwa kutumia kifaa kiitwacho Evaporation pan. Kivyovyote sehemu hii ya maji ya mvua hupotea bure. Japo kiasi cha maji haya kinachopotea huwa hakifahamiki na wapanga miundombinu wengi (infrastructure planners). Mfao angalia picha ya kwanza juu hapo, ni eneo la wazi bila hata miti pembeni wala uoto kitu ambacho ni kosa kubwa.

Mfumo wa mzunguko wa maji (Hydrological cycle)

Upotevu huu wa maji huwa kwa mfumo wa mvuke (water vapour), na mvuke hauonekani kwa macho ya kibinadamu (usiwaze ule mvuke kwenye sefuria unalopikia chakula baada ya kufunua mfuniko, la hasha fikiria eneo pana kama bwawa) hivyo huunda kiwango cha maji ambacho hupotea bila kujua  (unseen loss of water). Kutokana na hili, kiasi kikubwa cha maji hupotea katika mito,mabwawa, mitaro ya kugwia maji nakadharika.

Tazama mifano michache ya upotevu huu wa maji:
1.Fikiria eneo lenye ukubwa wa eneo 10KM2, na mvukizo katika uso wa eneo (Evaporation in vicinity of the reservoir) 5mm/siku.
Kiasi cha maji kinachopotea kwa siku (vizio vimebadilishwa vyote kweme mita kwaajili ya uzidishaji)    
= 5x 10-3 x 10 x 106 M2
=50,000M3
Kiasi hiki cha maji (mita za mraba 50,000) zinatosha kuhudumia kijiji chenye makazi (households) 300 kwa matmizi ya nyumbani (domestic water supply) kwa miaka sita (Lakini kinapotea kwa siku moja)

Au tazama mfano wa pili:
Fikiria eneo lenye maji kwa ukubwa wa 2KM2, na mvukizo katika uso wa eneo (Evaporation in vicinity of the reservoir) 5mm/siku.
Kiasi cha maji kinachopotea kwa siku (vizio vimebadilishwa vyote kweme mita kwaajili ya uzidishaji)    
= 5x 10-3 x 2 x 106 M2
=10,000M3
Kiasi hiki ch maji ni sawa na mvua au maji ya kumwagilia yenye kiwango cha milimita 100 kutumika katika shamba la hekta moja. Kwa lugha nyingine kiasi cha maji kinachopotea katika eneo la kuhifadhia lenye ukubwa wa kilometa mbili za eneo kwa siku moja kinatosha kutumika kumwagilia shamba lenye ukubwa wa hekta moja kwa mwaka mzima.

Kwa mifano hiyo miwili unaweza kupata picha ya haraka kiwango kikubwa cha maji kinachopotea kwa njia hii.

Nini kifanyike?
Mbinu za kupunguza upotevu huu wa maji zipo nyingi. Hapa nakutajia mbinu mbili rahisi kuzielewa

  1. Kwanza ni kuhifadhi maji katika miundombinu yenye kina kirefu kuliko eneo la juu ( greater depth than surface area). Hii inapunguza eneo la maji linalofikiwa na jua na upepo hivyo kupunguza mvukizo.

  1. Kupanda miti kuzunguka eneo ulilohifadhi maji kwa maana upepo pia huweza kuchangia mvukizo kwa kiwango fulani.

Kumbuka njia za upoteve wa maji katika mabwawa ziko nyingi na kila moja na njia yake ya kupunguza kwa maana sio rahisi kuthibiti kwa asilimia 100.
Tazama bwawa hili lilivyozungukwa na miti. Kwa njia hii mvukizo huwa kidogo sana na nirahisi kingo zake kutumika kama mazalia ya samaki na kuchochea uzalianaji wa ikolojia nyingine.


Nakupongeza kwa kujifunza na endapo unaswali juu ya mada hii waweza uliza kwa nia yoyote uipendayo. Like page yetu facebook pia (Water Droplet Community-WADCo Tanzania) kwa mada nyingine nyingi zinazohusu maji, umwagiliaji, udongo na mazingira. Naamini pia umeelewa kiswahili changu ambacho pengine baadhi ya maneno huwa rahisi kueleweka yakitumika kwa lugha ya kiingereza.

Eng Herman Nguki (Irrigation & Water Resources)

0763 639 101/0679 639 101
Follow instagram @eng.ngukiwamalekela
Nakukumbusha kwa mada mbalimbali za vijana, jamii,mahusiano na imani tembelea www.ngukiherman.blogspot.com

Thursday, February 16, 2017

MIGOGORO YA MAJI YAZIDI KUONGEZEKA


Ofisi za Bonde la Mto Pangani, mkoani Kilimanjaro, imekiri kuwapo kwa ongezeko kubwa la migogoro kati ya wakulima na wananchi wa kawaida inayosababishwa na uhaba wa maji.
Akizungumza na waandishi wa habari (5 Jan 2017), Ofisa wa Bonde hilo, Mtoi Kanyawana, alisema migogoro ya maji imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na ukame kuyakumba baadhi ya maeneo nchini.
“Hadi sasa tumepokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali ikiwamo katika vijiji 19 vya Wilaya ya Moshi, mkoani hapa vyenye wakazi zaidi ya 56,000.
“Wananchi hao wanadai kukosa huduma ya maji ya kunywa na matumizi ya nyumbani kutokana na uwepo wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Kirua Kahe.
“Changamoto kubwa inayosababisha vyanzo vingi vya maji kuvamiwa na kuharibiwa vibaya na wananchi ni kutokana na kubadilika badilika kwa uongozi wa maeneo ya vijiji, hali ambayo inasababisha mfumo wa matumzi ya maji kubadilika.
“Hata hivyo, kwa sasa tupo katika mchakato wa kuainisha na kuyapandisha hadhi baadhi ya maeneo ya vyanzo vya maji na kuyahifadhi ili kuhakikisha vyanzo hivyo vinalindwa na tatizo la upungufu wa maji linakwisha,” alisema Kanyawana.
Kwa mujibu wa Kanyawana, maeneo yote ambayo yanategemewa kupandishwa hadhi na kuwa hifadhi, yatakuwa chini ya miliki ya bonde hilo na jukumu la kusimamia maeneo hayo wataliacha kwa Serikali za mitaa na vijiji kwa kushirikiana na jumuiya za watumia maji.
“Yapo maeneo ambayo ni vyanzo vya maji, tuna mpango wa kuja kuyatangaza ili yajulikane rasmi ili wananchi ikiwamo wafugaji ambao wataingia, waweze kuwajibishwa kisheria.
“Lakini pia, maeneo mengine ambayo yana vyanzo vya maji husimamiwa na jumuiya za watumia maji ambazo zipo kisheria,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema suala la utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji ni jambo muhimu na si jukumu la ofisi za Bonde la Mto Pangani peke yake.

Source// Mtanzania 6 Jan 2017
Bila maji hakuna watu. Hayana ladha lakini huishi tabasamu wakati wa kuyanywa.

Kwa sisi wadau wa rasilimali maji lazima tukubali kuwa hali hii inakoelekea inazidi kuwa mbaya. Nimechukua habari hiyo ya mfano kwa mkoa wa Kilimanjaro, lakini hali ni tete sehemu nyingi sana za nchi yetu. Hapa hatujikiti tu kulaumiana lakini upungufu wa maji maeneo mengi umetokana na uharibifu wa mazingira, uvamizi wa vyanzo vya maji kwa kilimo n.k. Kwa bahati mbaya wavamizi wa vyanzo vya maji wamekuwa wakifumbiwa macho ilihali wanafahamika, na huenda ni watu wenye ushawishi kwa jamii au nyadhifa fulani.
Lazima jicho la tatu litumike kuangalia tunakoenda. Mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo nayo kwa kiwango kikubwa yamechagizwa na uharibifu wa mazingira yanatishia hali ya maisha ya kizazi kijacho. Ni kweli teknolojia nyingi zinazidi kuvumbuliwa ili kutumia nishati mbadala na rafiki kwa mazingira, lakini bado muamko wa jamii ni mdogo ama kutokana na ukosefu wa elimu, gharama za teknolojia au makusudi tu.
Hili lipo wazi na ndio maana ukienda baadhi ya maeneo ambako wametunza mazingira na wamejiwekea sheria kali za kuthibiti wahalibifu wa misitu na wavamizi wa vyanzo vya maji, hali ni nzuri sana kana kwamba wao sio wa nchi hii. Kumbe jamii sasa umefika wakati wa kubadilika na kuthamini mustakabali wa kizazi kijacho. Sio tu kuweka sheria, bali kuwa na ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha hakuna anayekiuka. Bila maji hakunamaisha.
Eng Nguki Herman (Rasilimali maji na umwagiliaji)
0763 639 101/0679 639 101
ngukiherman@ymail.com


Asante kwa kutembelea blog yetu. Kwa maoni na ushauri au maswali usisite kutuandikia kupita mawasiliano yaliyopo au kwa njia ya comment. Karibu pia www.ngukiherman.blogspot.com kwa mada mbalimbali za viajana, ushauri , familia na maisha kwa ujumla.